
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI KIKOMO ZA BIDHAA ZA MAFUTA YA PETROLI KUANZIA JUMATANO, TAREHE 6 AGOSTI 2025
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zitakazotumika kuanzia Jumatano ya tarehe 6 Agosti 2025 saa 6:01 usiku.
Kwa mwezi Agosti 2025, bei za rejareja na za jumla katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ni kama zinavyoonekana katika Jedwali Na. 1 na 2, mtawalia.
MWENENDO WA BEI ZA MAFUTA YALIYOSAFISHWA KATIKA SOKO LA DUNIA
- Bei za mafuta hapa nchini zinazingatia gharama za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la Uarabuni. Katika bei kikomo kwa Agosti 2025, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 2.3 kwa mafuta ya petroli, zimeongezeka kwa asilimia 5.5 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.7 kwa mafuta ya taa.
MWENENDO WA GHARAMA ZA UAGIZAJI
- Kwa mwezi Agosti 2025, gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 12.43 kwa mafuta ya petroli, asilimia 3.11 kwa mafuta ya dizeli na kuongezeka kwa asilimia 13.08 kwa mafuta ya taa; katika Bandari ya Tanga hakuna mabadiliko; na zimeongezeka kwa asilimia 6.12 kwa mafuta ya petroli na asilimia 60.82 kwa mafuta ya dizeli katika Bandari ya Mtwara.
VIWANGO VYA KUBADILISHA FEDHA ZA KIGENI
Gharama za mafuta (FOB) na gharama za uagizaji (Premiums) zinalipiwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani. Kwa bei za mwezi Agosti 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) umepungua kwa asilimia 2.
Wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa rejareja wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei zinazooneshwa katika Jedwali Na. 3. Aidha, wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei zinazooneshwa katika Jedwali Na. 2. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakayekiuka AGIZO hili.
EWURA inapenda kuwakumbusha wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja pamoja na jamii kuzingatia yafuatayo:
- Bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.
- Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.
- Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo (Price cap) au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price) kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022 zilizotangazwa tarehe 28 Januari 2022 kupitia Gazeti la Serikali Na. 57 na marekebisho ya Kanuni tajwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 761A la tarehe 30 Oktoba 2023 na Mabadiliko ya Kanuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja za Mwaka 2024.
- Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.
- Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita. Stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa. Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli.
Bei Kikomo Za Bidhaa Za Mafuta ya Petroli Kuanzia Jumatano, Tarehe 6 Agosti 2025.