Vital’O Yapania Kuitoa Yanga Sc Klabu Bingwa Afrika
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu ya Vital’O ya Burundi, Arsene Bucuti amesema wamekuja nchini kuitoa Yanga SC katika Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.
Vital’O imepangwa kucheza na Yanga SC katika Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na mchezo huo utafanyika Jumamosi katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Arsene alisema wanaiheshimu Yanga SC, lakini hiyo haiwafanyi waihofie na wamekuja Tanzania kwa ajili ya kazi hiyo ya kuwatoa kwa kuwa wameifuatilia vyema.
“ Tumekuja hapa kwa kazi moja tu. Kuwatoa Yanga SC. Tuna kila kitu ambacho wao wameshinda. Hatutishiko nao.
“ Tumewafuatilia katika michezo yote ambayo wamecheza kule Afrika Kusini hadi hapa Tanzania, hivyo tunaenda kucheza na timu tunayoifahamu vyema “ alisema Arsene.
Arsene aliongeza kuwa Yanga SC ina mashabiki wengi Burundi kutokana na wachezaji Ammis Tambwe, Saidoo Ntibazonkiza na Didier Kavumbagu kuwahi kuitumikia timu hiyo.
Michezo hiyo miwili ya nyumbani na ugenini ya Yanga SC dhidi ya timu hiyo itachezwa nchini Tanzania kutokana na Burundi kukosa uwanja wenye sifa ya kutumika katika mechi za CAF.